Kama ilivyo katika mila za mataifa na makabila yote. Nitaongelea kuhusu mila ya ndoa za wanyisanzu. Kwa vile sijapata muda wa kuwapata wazee wenyewe wanielezee zile za asili zilikuwaje. Natarajia wadau wangu wanaoelewa watanisaidia kwenye maoni. Kwa miaka ya sasa haiangalii sana unaolewa na mtu anayetoka kabila au ukoo gani.
Kwa simulizi toka kwa mama yangu. Zamani ilikuwa kijana akimpenda msichana, basi alitoa taarifa. Huyo binti alifuatiliwa ukoo wake kwa karibu kuangalia kama ukoo ule wana tabia gani, je wana magonjwa ya kurithi n.k. Endapo atakubalika basi alitafutwa mshenga wa kwenda kwa familia ya msichana. Huko walipangiwa jinsi ya familia hizi watakavyokuja na waje vipi na nini. Mahari (kinyanzala) ilipangwa kama ni ngombe wangapi na mazao kiasi gani.
Baada ya kufuata taratibu hizi, baada ya kuingia dini, ndoa ilifungwa kanisani kwa wakristo. Sitaongelea dini zingine na wapagani kwani sina taarifa sana. Kumbukumbu zangu za utotoni, nilishuhudia maharusi wakitupiwa maua toka kanisani wakitembea kwa miguu na kuimbiwa nyimbo za kuwasifu n.k.
Watu walikuwa wakarimu, hakukuwa na kadi za mualiko wala meza kuu. Nyumbani kuliandaliwa makande ya mtama(mpeke). Kinywaji kilikuwa togwa ya mtama na pombe. Ng'ombe alichinjwa na nyama kuliwa. Ngoma zilichezwa na wana kijiji walifurahi.